Wabunge CUF wasusia Baraza la Wawakilishi



MAWAZIRI na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitia Chama cha Wananchi (CUF), jana walitoka ndani ya Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi mjini hapa, wakati Mwakilishi wa Jimbo la Bububu, Hussein Ibrahim Makungu (CCM), alipokuwa akiapa.

Mawaziri na wabunge hao kupitia CUF, walitoka nje ya ukumbi huo jana asubuhi, baada ya Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, kutoa taarifa ya kuapishwa kwa mwakilishi mpya na kutaja jina la Hussein Ibrahim Makungu.

Baada ya Spika Kificho kutaja jina la Makungu, wawakilishi kupitia CUF, walitoka nje ya ukumbi kwa kile kilichoelezwa kuwa, hawakubaliani na ushindi wa Makungu, kwa kuwa uchaguzi uliomweka madarakani hivi karibuni, ulikuwa na utata.

Pamoja na CUF kususia tukio hilo, Makungu aliapishwa.

Makungu alipoapa, baadaye alizungumza na waandishi wa habari nje ya Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi ulioko Chukwani, nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Katika mazungumzo yake, Makungu alisema kwa sasa, ameapishwa rasmi na wananchi wa jimbo lake wakae tayari kwa maendeleo, kwani atatimiza ahadi zote alizoahidi wakati wa kampeni.

Akizungumzia kitendo cha wajumbe wa CUF kutoka nje wakati wa kuapishwa kwake, alisema hatishwi na tukio hilo, kwa kuwa anaamini alichaguliwa kihalali na wananchi wa Bububu.

“Kiukweli wenzetu wameonyesha hali ambayo si nzuri, lakini hata hivyo sisi CCM tumeliona hilo na tumejua wenzetu wapo katika mstakabali gani,” alisema Makungu kwa kifupi.

Akizungumza na MTANZANIA, Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani katika baraza hilo, ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Chonga, Abdalla Juma, alisema yeye na wenzake, walilazimika kutoka nje ya ukumbi kwa kuwa hawamtambui Makungu kama mshindi wa Jimbo la Bububu.

“Sisi hatumtambui Hussein Ibrahim Makungu, kuwa ni Mwakilishi wa Jimbo la Bububu, mpaka hapo Mahakama itakapotoa maamuzi yake, kwa sababu tumefungua kesi mahakamani kupinga ushindi wake.

“Hatumtambui kwa sababu wengi wetu tuliushuhudia uchaguzi mdogo uliomweka madarakani, uchaguzi huo ulijaa udanganyifu wa waziwazi na kulikuwa na utumiaji mkubwa wa nguvu za vyombo vya ulinzi, vilivyokuwa vikiibeba CCM. Pia Tume ya Taifa ya Uchaguzi, iliibeba wazi wazi CCM, kwa hiyo, hatuwezi kukubali ushindi wake, hadi hapo mahakama itakapoamua.

“Kwa maana hiyo, kama sisi tungeendelea kuwapo pale ukumbini, ingeonyesha kuwa tumeridhia kuwa Makungu ni Mwakilishi halali wa Bububu, kitu ambacho tunapingana nacho kwa asilimia zote

“Sasa basi, kitendo cha sisi kutoka ukumbini kwa upande mwingine, kitaionyesha Serikali Kuu, kwamba kuna mambo ambayo hayaendi vizuri kwa watendaji wake,” alisema Juma

Imeandikwa na Mtanzania Alhamisi, Octoba 11, 2012 (na Grace Shitundu), Zanzibar



Responses

0 Respones to "Wabunge CUF wasusia Baraza la Wawakilishi"

Post a Comment

 

Recent Comments

Popular Posts

Return to top of page Copyright © 2010 | Platinum Theme Converted into Blogger Template by HackTutors